Andiko: Mathayo 6:28–30: “Na mavazi, ya nini kuyahangaikia? Fikirini maua ya mashamba jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti; nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo.”
“Ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa motoni, je, hatawavika ninyi zaidi, enyi wa imani haba?”
Ninaomba maisha yenu yajazwe upendo na baraka za Mungu, na ningependa kushiriki nanyi neema kupitia ujumbe wenye kichwa “Ndoto Yenye Thamani ya Kweli.” Methali moja husema, “Mtu asiye na ndoto huwa mtumwa wa mwenye ndoto.” Haidhuru mtu ana ujuzi kiasi gani; asipokuwa na maono ya wakati ujao, anaweza kufanya kazi tu kwa ajili ya mtu mwenye maono.
Kwa hiyo, ni muhimu sana kushikilia ndoto zako, lakini muhimu zaidi ni kufahamu ndoto zako ni za aina gani. Wengine hutumia muda na nguvu zao zote ili kuishi maisha ya utajiri, wengine hujikusanyia maarifa mengi kadiri iwezekanavyo, na wengine hutafuta heshima. Je, watu wanaweza kuridhika wanapotimiza ndoto zao?
Sulemani alikuwa mfalme wa Israeli ya kale. Alikuwa miongoni mwa watu waliopata utajiri na heshima nyingi zaidi katika historia. Alikuwa na ufahamu wa kila jambo kupitia hekima ambayo hakuna mtu aliyewahi kupewa kabla yake, wala baada yake. Nchi yake ilistawi sana kiasi kwamba wafalme wa nchi jirani waliionea wivu hekima, ufahamu na heshima aliyokuwa amepewa.
Hata hivyo, mwishoni mwa maisha yake alikiri, “Ubatili mtupu! Ubatili mtupu! Yote ni ubatili. Mwanadamu ana faida gani katika kazi yake yote anayoifanya chini ya jua? Jumla ya mambo yote, baada ya kusikilizwa, ni hii: mche Mungu na uzishike amri zake, maana ndiyo impasayo kila mtu.” Unapaswa kukumbuka kwamba ndoto inayoturidhisha kweli na kudhihirisha thamani yake ya kweli milele hutimizwa ndani ya Mungu Muumba, ambaye ndiye Bwana wa roho zetu. Kwa hiyo, panda moyoni ndoto zinazofaa na zinazoweza kuthibitishwa na Mungu.
Mungu wa upendo aliwaumba wanadamu na akaanza kuwalea ili apate watoto wa kweli ambao ataweza kushiriki nao upendo usiobadilika milele. Watu wengine hawaujui moyo wa Mungu, na kwa sababu ya dhambi hufuata njia ya mauti. Wengine hutambua na kushukuru kwa upendo mkuu wa Mungu, nao huwa watoto wake wa kweli wanaomfanana. Ndiyo maana Mungu amekuwa mvumilivu—siku moja kwake ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja—na anaendelea kuvumilia hata leo.
Wakati wake utakapofika, atakusanya ngano nzuri ghalani; yaani, atawakusanya watoto wake katika Ufalme wa Mbinguni. Kadiri watoto wake wanavyotakasa na kusafisha mioyo yao, ndivyo Mungu atakavyowakaribisha zaidi kwenye kiti chake cha enzi na kushiriki nao upendo wake milele. Kwa hiyo, kila siku jichunguze kwa Neno la Mungu, badilika uwe mtu wa kweli na umfanane Kristo moyoni. Ninaomba kila mmoja wenu awe mtoto wa kweli wa Mungu mwenye ndoto zenye maana na tumaini la kuingia Yerusalemu Mpya. Ninaomba haya katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo!
His Emeritus Bishop Dr. Jaerock Lee
Kwa nini Yesu, Mwana wa Mungu, alisema alikuwa na kiu? Adhabu ya kusulubiwa ilikuwa ya kutisha sana hivi kwamba mtu mwenye mwili aliponing’inizwa msalabani, hangeweza kufanya lolote ila kuvumilia maumivu makali na kiu isiyovumilika.
Mfalme na maafisa wake walimwacha Mungu na kuabudu sanamu. Ghadhabu ya Mungu ikawajia watu wa Yuda, nao wakavamiwa na jeshi la Waaramu.
Upendo hautafuti faida yake mwenyewe, bali hujitoa kwa ajili ya wengine. Huo ndio upendo wa kweli wa kiroho usiobadilika milele. Mungu anataka tuishi katika wema na haki, na kuitimiza Sheria kwa upendo.